Tuesday, July 14, 2009

MICHE BORA YA MATUNDA ILIYOBEBESHWA

Umuhimu wa Miche Bora ya Matunda iliyobebeshwa Katika Kupunguza Umaskini

Matumizi ya miche bora iliyobebeshwa kwa kilimo cha matunda ni moja ya teknolojia muhimu itakayowawezesha wakulima kuongeza tija na kujikwamua kutoka katika umaskini.

Haya yanatokana na ukweli kwamba, miche iliyobebeshwa kitaalam huzaa matunda bora na mapema na hivyo humhakikishia mkulima mavuno bora na kipato cha haraka kuliko miche ya kienyeji.

Hayo yalisemwa na Afisa Kilimo Mwandamizi Bi. Judith Kitivo, mtaalam wa mazao ya bustani alipotembelewa ofisini kwake hivi karibuni.

Aidha, ubebeshaji wa miche ya matunda hufanywa kwa mazao ya jamii moja kwa mfano limau na aina nyingine ya limau, limau na chungwa au aina moja ya parachichi na nyingine alisema Bi Kitivo.

Hata hivyo, alizitaja faida nyingi zitokanazo na ubebeshaji wa miche zikiwa ni pamoja na kuharakisha uzaaji wa matunda kutokana na kukomaa kwa kikonyo kinachotumika, kudhibiti magonjwa na wadudu walioko udongoni, kupata miche yenye sifa nzuri, kuzalisha mazao miti (woody plants) ambayo hayawezi kuzalishwa kwa vipande (cuttings) pamoja na kuweza kuzalisha aina tofauti za mazao kama machungwa na limau katika mti au mmea mmoja; alisema mtaalam huyo.

Mbali na hayo alisema zipo aina mbili za ubebeshaji, ambazo ni ule wa kishina na kitawi /kikonyo (grafting) ambao hufanyika kwa uzalishaji wa miche kama miembe na miparachichi; na aina ya kishina na jicho la kikonyo (budding) ambao hufanyika kwa uzalishaji wa miche jamii za michungwa.

No comments:

Post a Comment